Marekani yasema kuwa Korea Kaskazini ilikusudia kufanya uchokozi........


Marekani imesema Korea Kaskazini ilikuwa na nia fulani ilipotekeleza jaribio la kombora ambalo lilifeli mwishoni mwa wiki.
Waziri wa Ulinzi James Mattis amesema jaribio hilo lilikuwa la kutojali na kwamba Marekani "inafanya kazi kwa karibu" na China kukabiliana na Korea Kaskazini.
Amesema Korea Kaskazini ilifanya hivyo ikikusudia kufanya "uchokozi fulani".
Marekani ilisema kombora hilo la Korea Kaskazini lilipuka muda mfupi baada ya kurushwa angani.
Pyongyang imesema inaweza kuwa ikifanyia majaribio makombora kila wiki na pia ikaonya kwamba kutatokea "vita kamili" iwapo Marekani itaichukulia hatua za kijeshi.
Iwapo Marekani wanapanga kutushambulia, tutajibu kwa shambulio la nyuklia kwa mtindo na njia yetu wenyewe," naibu waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini Han Song-ryol aliambia BBC Jumatatu.
Pande zote mbili zimekuwa zikijibizana vikali baada ya Korea Kaskazini kufanya jaribio hilo la makombora.
Bw Mattis alisema kwamba jaribio hilo la Jumapili halikuhusisha kombora linaloweza kuruka kutoka bara moja hadi jingine lakini bado lilikuwa ishara ya kutojali.
"Inadhihirisha ni kwa nini tunafanya kazi kwa karibu kwa sasa na Wachina...tunajaribu kudhibiti hali hii na lengo letu ni kumaliza silaha za nyuklia katika rasi ya Korea," alisema. Chanzo bbc swahili

Comments