Vikwazo kwa Makamu wa Rais Venezuela


Marekani imetangaza vikwazo dhidi ya Makamu wa Rais wa venezuela Tareck El Aissami kwa tuhuma za kuhusika na ulanguzi wa kimataifa wa mihadarati. Bwana El Aissami ameongezwa kwenye orodha ya walanguzi wakuu wanaosakwa na Marekani.
Pia bwenyenye maarufu wa Venezuela Samark Lopez pia amewekewa vikwazo kwa kutuhumiwa kama mshirika mkuu wa El Aissami. Tareck El Aissami aliteuliwa kama Makamu wa Rais na Rais Nicolas Maduro mwezi uliopita.
Amekanusha madai ya kuhusika na visa vyovyote ya jinai. Bwana Lopez hajajibu hatua hizi za Marekani. Vikwazo hivi vinamaanisha kwamba mali yote ya Makamu wa Rais iliyoko Marekani inapigwa tanji huku akizuiwa kuingia nchini humo.
Wizara ya fedha ya Marekani imesema bwana El Aissami alisimamia kuvukishwa kwa tani nyingi za mihadarati ndani ya Marekani kwa kutumia ndege au meli. Aidha imeongeza alikua kwenye orodha ya waliopokea mulungula kutoka kwa mlanguzi mkuu wa mihadarati wa Venezuela aliyeko korokoroni Walid Makled, ili kumkinga wakati akiendelea na biashara haramu.

Bwana El Aissami aliwahi kuwa gavana wa jimbo la Aragua na pia akawa waziri wa ndani na sheria nchini Venezuela kati ya mwaka 2008 na 2012. Taarifa zilizonadiwa na mashirika ya habari Marekani zinasema bwana El Aissami alikua akichunguzwa na Marekani kwa kushirikiana na kundi la wapiganaji la Hezbollah nchini Lebanon.
Wakati akiwa waziri wa ndani imedaiwa pasipoti kadhaa za Venezuela zilipatikana zikitumiwa na wapiganaji wa Hezbollah. Mapema mwezi huu wabunge 34 wa baraza la Congress Marekani walimuandikia waraka Rais Donald Trump wakimtaka kuweka vikwazo kwa baadhi ya maafisa wa serikali ya Venezuela.
Walimtaja hasa Tereck Al Aissami wakisema ana nafasi kubwa ya kuongoza nchi kama Makamu wa Rais na alistahili kuchukuliwa hatua kutokana na tuhuma zake kuhusika na ulanguzi wa mihadarati pamoja na kuwa mshirika wa kundi ambalo Marekani imeliorodhesha kama la kigaidi. Chanzo BBC Swahili..... 

Comments