TBS na Madereva nani Mkweli?



Wakizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoandaliwa na mabalozi wa usalama barabarani (RSA), madereva hao wameitupia lawama TBS wakidai ndiyo chanzo cha magari kupata ajali.

Dar es Salaam. Madereva wa mabasi yaendayo mikoani wamelitupia lawama Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuruhusu matairi ya magari yasiyokuwa na viwango yaingizwe hapa nchini.
Wakizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoandaliwa na mabalozi wa usalama barabarani (RSA), madereva hao wameitupia lawama TBS wakidai ndiyo chanzo cha magari kupata ajali.
Dereva, Athumani Abdallah amesema wanashangaa wao kulalamikiwa kuwa ndiyo chanzo cha ajali wakati adui wao ni TBS ambayo inafanya ukaguzi wa ubora wa matairi.
Amesema idadi kubwa ya ajali za barabarani husababishwa na matairi kupasuka hivyo gari kupoteza mwelekeo.
Mkurugenzi wa RSA, Mallin Komba amesema madereva wanatakiwa kufahamu wajibu wao na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali nchini.
“Kazi yetu ni kutoa elimu kwenye vituo vya mabasi ya mikoani kila siku asubuhi kabla ya safari kuanza,” amesema  Komba.
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Profesa Egid Mubofu amesema shirika hilo haliwezi kupitisha matairi yaliyo chini ya kiwango kwa sababu linavisimamia vilivyowekwa kitaifa.
“Hizi tuhuma si za kweli hakuna uchochoro wowote unaotumika, kama wana ushahidi watuletee. Sisi tunafanya kazi kwa kufuata viwango vilivyowekwa,”amesema Profesa Mubofu.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga akitoa takwimu za ajali za barabarani mwaka 2016 amesema vifo vya madereva vilikuwa 242, watembea kwa miguu 992 na abiria 1,009.
Mpinga amesema kwa upande wa majeruhi madereva walikuwa 607, watembea kwa miguu 1,640 na abiria 4,650. Chanzo Mwananchi

Comments